Yanga: Hatumlazimishi Ngoma

Imeandikwa na Mohamed Akida

UONGOZI wa Yanga umesema hauwezi kumlazimisha mshambuliaji wake Donald Ngoma kucheza kama yeye mwenyewe hayupo tayari na ripoti ya daktari wa timu inasema mgonjwa.

Kwa muda mrefu kiasi Ngoma hajaichezea Yanga kukiwa na tetesi mbalimbali juu ya hilo kabla ya juzi kuibuka na tuhuma dhidi ya Daktari Haroun Haroun, akidai ripoti yake inamgombanisha na mashabiki na viongozi wa Yanga, kwa vile inadai amepona huku ile ya daktari wa Yanga, Edward Kibavu ikisema mgonjwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa alisema uongozi hauwezi kuingilia suala hilo kwa vile kuna wataalamu wa afya wameajiriwa kwa ajili ya kufuatilia afya za wachezaji.

“Unajua Yanga inahitaji watu wanaowajibika kwenye majukumu yao… siwezi kusema kama anaumwa au la, kucheza kwake itategemea na yeye mwenyewe na ripoti ya kocha,” alisema.

Ngoma inadaiwa anasumbuliwa na nyonga, lakini daktari aliyekabidhiwa kwake Haroun anasema mchezaji huyo yupo fiti na ni vyema akawaeleza ukweli kinachomfanya ashindwe kuitumikia timu hiyo.

Ripoti ya daktari wa timu ya Yanga Bavu, inadai Ngoma ni mgonjwa na anatakiwa kuwa nje ya dimba kwa miezi mitatu ili kupona tatizo hilo ambalo limemweka nje kwa muda mrefu bila kuitumikia timu yake.

Mkwasa alikiri kupokea ripoti ya Daktari Bavu, inayomtaka mchezaji huyo kuwa nje kwa kipindi hicho na kusema hawana namna kwa sababu wanaheshimu ripoti ya daktari na mchezaji mwenyewe.

“Ni kweli nimepokea ripoti ya Bavu, inayosema Ngoma bado ni mgonjwa na atakuwa nje kwa miezi mitatu, sisi kama uongozi hatuna namna isipokuwa mchezaji mwenyewe kama atajiona yupo sawa na kutaka kuitumikia timu sawa vinginevyo hatuwezi kumlazimisha, ni vigumu kumlazimisha,” alisema Mkwasa.

Awali Daktari Haroun aliyepewa kazi ya kumtibu Ngoma na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji (hataki kumtaja jina) baada ya kutoka kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi alisema alimtibu mchezaji huyo kwa wiki mbili jeraha la goti na kupona kabisa na mchezaji huyo aliweza kucheza mechi ya ligi dhidi ya Stand United Februari 3, lakini mchezaji huyo hakumaliza mchezo huo akaumia na kushindwa kuendelea na mchezo.

Alisema baada ya mchezo alimtafuta Ngoma kwa simu na kumuuliza bado goti linamsumbua mshambuliaji huyo akamjibu kuwa siyo goti bali ni nyonga na akamuahidi kumsaidia tena na alifanya hivyo baada ya kumpatia matibabu mchezaji huyo alisema amepona lakini hata vipimo alivyomfanyia kwa matatizo ya nyonga havikuonesha kama kuna tatizo.

“Kitaalamu kuna aina nne ya matibabu katika mpira, kuna sports medicine doctor, physiotherapy, sport nutrition advisor na chiropractor ambayo tunaita matibabu mkandamizo utaalamu huu nchi yetu Hakuna, Ngoma aliwaongopea viongozi wa Yanga kwa kuja na ripoti ya kutengenezwa kutoka London Health ambayo imeandikwa na Physiotherapy na siyo daktari wa Michezo.

Ngoma juzi alisikika kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwa ameamua kuweka wazi tatizo linalomfanya kuwa nje kwa muda mrefu kuwa ni Daktari Haroun, ambaye ameshindwa kumtibu licha ya kupewa fedha za matibabu na uongozi wa timu na mara zote lawama zimekuwa zikishishushwa kwake kuwa amechoka kuitumikia timu hiyo na anataka kuondoka kitu ambacho siyo kweli.

Mchezaji huyo alisema ataweka wazi hatima yake Yanga.

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*