Rais Magufuli, Lissu walivyobadili upepo uchaguzi wa TLS

Dar es Salaam. Kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kuchukua fomu ya kuwania urais ndani ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na angalizo la Rais John Magufuli kwamba taasisi hiyo ya kitaaluma isigeuzwe kuwa ya kisiasa, kimeufanya uchaguzi wa viongozi wa wanasheria hao mwezi ujao kuwa na msisimko wa aina yake.

Baada ya kauli hiyo ya Rais Magufuli ambayo ilifuatiwa na ile ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ya kutishia kukifuta chama hicho kama kitajihusisha na masuala ya kisiasa, wanasheria na wanasiasa walijitokeza kupinga wakiitaka Serikali isiingilie uchaguzi huo.

Misuguano hiyo imewafanya si wanasheria, wasomi na wadau wa masuala ya sheria pekee, kufuatilia kinachoendelea ndani ya TLS na uchaguzi huo, bali wananchi kwa ujumla hivyo kuufanya kuwa na msisimko mkubwa tofauti na mwingine wowote uliowahi kufanyika pengine tangu kilipoanzishwa mwaka 1954.

Kabla ya Rais kutoa angalizo hilo, mchakato wa uchaguzi huo ikiwamo waliochukua fomu haukuwa umewekwa wazi lakini baada ya ‘kuzinduliwa’ ufuatiliaji ulikuwa mkubwa hasa baada ya kamati ya uchaguzi ya TLS kupitisha majina matano ya wanaowania urais.

Mbali ya Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, wengine waliojitokeza kugombea nafasi hiyo ni kada wa Chadema ambaye kabla ya kujiunga na chama hicho alikuwa Mbunge wa Nyamagana (CCM) na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha. Pia yumo aliyewahi kuwa Rais wa TLS katika ya mwaka 2011 hadi 2013, Francis Stolla, Godwin Mwapongo na Victoria Mandari.

Uchaguzi wa TLS unatarajiwa kufanyika Machi 18 na mawakili 6,000 watapiga kura na kumpata mrithi wa Rais wa sasa John Seka.

Awali, Lissu alisema ameamua kuwania nafasi hiyo kutokana na Rais Magufuli kusema kuna kampeni zinazoendeshwa na chama fulani (hakukitaja) kwenye uchaguzi huo wa TLS.

Pia, Lissu alisema kauli ya Rais ya kwamba mawakili wanaowatetea wauza dawa za kulevya wakamatwe imemfanya agombee ili kulinda Katiba na sheria za nchi.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu mrengo wake wa kisiasa, Lissu alisema masuala ya kisheria hayana uhusiano na vyama vya siasa na kwamba jukumu la chama hicho ni kulinda katiba na sheria.

“Sigombei ili kupeleka Chadema ndani ya TLS. Masuala haya yanatuhusu sisi wote kujua mambo yanapoharibika, kuona sheria zinapokiukwa na kuona sheria mbovu zinapotungwa,” alisema alipohojiwa na mwandishi wetu.

Upepo huo ulibadilika zaidi baada ya Dk Mwakyembe kutoa tishio la kuifungia TLS ikiwa itajihusisha na siasa.

Dk Mwakyembe katika tamko lake ambalo wadadisi wa masuala ya kisiasa wanadai kwamba lililenga kukionya chama hicho kuhusu wagombea ambao pia ni wanasiasa, alisema ikiwa kimeamua kubadili mwelekeo, kiende kwa Msajili wa Vyama Siasa ili kisajiliwe rasmi la sivyo atapeleka bungeni mapendekezo ya kufuta sheria iliyokianzisha.

Kauli hiyo mbali ya kupingwa vikali ndani ya nchi, hivi karibuni, Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS) kilimwandikia barua Dk Mwakyembe kikimtaka aache kuingilia uchaguzi huo kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria.

Barua hiyo ambayo iliandikwa na Rais wa EALS, Richard Mugisha ilisema TLS si chama cha kisiasa na kimeanzishwa kwa kufuata taratibu zote.

Maoni ya wanasheria

Alipoulizwa maoni yake kuhusu uchaguzi huo, Wakili wa kujitegemea, Methew Kakamba alisema umekuwa gumzo kutokana na kauli za baadhi ya wagombea akiwamo Lissu aliyedai kuwa ameamua kuwania nafasi hiyo kutokana na kile alichokisema Rais Magufuli juu ya TLS.

“Lissu siyo mwanasheria tu, ni mbunge sasa anapotamka kauli zinazomtaja mkuu wa nchi (Rais), watu wanafuatilia kwa ukaribu zaidi,” alisema akizungumzia sababu za uchaguzi wa mwaka huu ndani ya chama hicho kuwa na msisimko mkubwa zaidi.

Alisema itikadi za chama hazimfanyi mtu kukosa vigezo kwa kuwa ni haki yake kikatiba na kwamba hata yeye ni kada wa CCM licha ya kuwa wakili hivyo demokrasia inabidi ifuatwe.

Mwanasheria mwingine, Thomas Msasa alisema baada ya wagombea ambao ni maarufu na nguli katika siasa kugombea, kumeongeza hamasa zaidi tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita.

“Katiba inatupa uhuru, uchaguzi ufanyike kwa haki bila kujali vyama. Tunahitaji Rais ambaye anaweza kutetea masilahi ya mawakili na siyo ya vyama vya siasa wala matakwa yake,” alisema Msasa.

Wakili Josephat Kasegero alisema uchaguzi wa mwaka huu umeonekana kuwa na mvuto kutokana na jinsi Lissu anavyopambana na Serikali katika masuala mbalimbali akisema yumkini hiyo ndiyo sababu ya Rais Magufuli na Dk Mwakyembe kutoa matamko hayo.

“Lissu ni mwanasheria wa kawaida lakini kwa wakati huu ameonekana akipambana sana na kuipinga Serikali ndiyo maana inakuwa hivyo,” alisema Kasegero.

Alisema katika kinyang’anyiro hicho mwanasiasa si Lissu pekee, bali yuko Masha na wanaompinga wanadhani kwamba anaweza kuingiza siasa kwenye chama cha kitaaluma.

Kampeni zaendelea

Wakati danadana hizo za kisheria na kisiasa zikitawala kuelekea uchaguzi huo, kampeni za kuwania nafasi hiyo zinaendelea licha ya kwamba hakuna utaratibu maalumu wa uratibu.

Ofisa Maboresho ya Sheria wa TLS, Mackphason Buberwa alisema hadi sasa hakuna mabadiliko wala malalamiko yaliyowasilishwa kwa chama hicho na kampeni zinaendelea kama kawaida.

“Sisi kama sekretarieti hatuhusiki na kupanga utaratibu lakini kuna majukwaani wanayotumia kuendesha shughuli hizo,” alisema.

(Chanzo-Mwananchi)

78 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*