Hospitali ya Haydom kupandishwa hadhi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali haina kipingamizi cha kuipandisha hadhi Hospitali ya Rufaa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri ya Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara kuwa hospitali ya kanda.

Amesema kwa kuipandisha hadhi itaipunguzia gharama serikali ya kuwahudumia wagonjwa kutoka mikoa jirani ya Arusha, Singida na Dodoma.

Aliyasema hayo jana alipotembelea hospitali hiyo ambako alipata nafasi ya kuzungumza na watumishi wa hospitali pamoja na kufanya mkutano wa hadhara, ambako alisisitiza kuwa amefarijika kuona huduma zinazotolewa.

Waziri Mkuu alisema ili kufikia vigezo vinavyokubalika kupandishwa hadhi kuwa ya kanda, amemwagiza Waziri wa Afya kuitembelea hospitali hiyo na kufanya mapitio ya kitaalamu na kujiridhisha ili taarifa rasmi itolewe na kufanyiwa kazi, ikiwamo kuangalia kuwa na vifaa vya kutosha.

“Serikali itaendelea kuheshimu na kuthamini mchango mkubwa wa Hospitali ya Hydom katika kuwahudumia watu na itaendelea kusaidiana katika kutatua kero mbalimbali za tiba kwa sababu wagonjwa hao tungehangaika nao katika hospitali za ngazi ya mkoa kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Singida,” alieleza Waziri Mkuu.

Alisisitiza kuwa hospitali hiyo ni ya Watanzania hivyo serikali imesikia kilio cha kuipandisha hadhi, hivyo muhimu ikaimarishwa na kwamba kero ya kufungua barabara za kutumiwa na wagonjwa hao zipitike kwa urahisi ambapo utekelezaji wake umekwisha anza Karatu-Mbulu-Hydom-Maswa kazi ya upembuzi wa awali imeshaanza.

Pamoja na kuimarisha vituo vya afya na zahanati nchini, alisema serikali imetenga fedha kwa mwaka huu wa fedha Sh bilioni 251 kwa ajili ya kununulia dawa kwa kuwa kumekuwa na kero nyingi za ukosefu wa dawa katika vituo vya afya, zahanati na hospitali za wilaya na mikoa.

Aidha, alisema serikali imeanza kuajiri watumishi mbalimbali katika nsekta za elimu ambapo walimu 4,396 wa masomo ya sayansi wameajiriwa ikiwa ni pamoja na kutarajia kuajiri watumishi wa afya zaidi ya 5,000 hadi 6,000 katika vituo vya afya, zahanati hospitali za wilaya na mkoa ikiwemo Hospitali ya Hydom.

Akitoa taarifa ya hospitali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba Hospitali ya Rufaa ya Hydom, Dk Emmanuel Nuwass aliiomba serikali kutoa kibali cha ajira ya jumla ya watumishi 90 ambao hospitali hiyo iliomba kupitia bajeti yake ya mwaka 2016/2017 na kuboreshewa kwa barabara kutoka Karatu, Mbulu, Hydom hadi Singida kwa kiwango cha lami ili wagonjwa wafike kwa urahisi.

Mmiliki wa hospitali hiyo, Askofu Nicolous Nsanganzelu alimshukuru Waziri Mkuu na serikali kwa kutambua mchango wa hospitali hiyo katika kuwahudumia wananchi, jambo ambalo alisisitiza limeongeza hamasa katika utafiti wa magonjwa yanayofanywa katika kituo cha utafiti hospitalini hapo na huduma za tiba.

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*