Lwandamina achimba mkwara mzito Yanga

Imeandikwa na Mohamed Akida

KOCHA mpya wa mabingwa wa soka wa Tanzania Bara Yanga, George Lwandamina amechimba mkwara mzito na kusema atakuwa mkali kwa wachezaji wazembe kwenye klabu hiyo.

Lwandamina alitangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa klabu hiyo na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Hans van Pluijm ambaye kwa sasa atakuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo.

Lwandamina aliliambia gazeti hili hivi jana kuwa atakuwa mkali kwa wachezaji wazembe kutokana na makubaliano aliyoingia na viongozi wa klabu hiyo ambayo alisema yanamlazimu kuwa mkali.

“Uongozi unataka ubingwa wa Ligi ya Mabingwa na kushinda kila taji hapa nchini, huu ni mtihani mkubwa kwangu lakini kama kocha nimeukubali kwa kuwa natambua Yanga ni timu kubwa na yenye wachezaji wanaojitambua,”alisema Lwandamina.

Alisema siku zote katika kazi yake ya ukocha amekuwa na mapenzi makubwa na wachezaji wake kwa sababu anaamini ndio watakaompa mafanikio na kusema katika hilo angependa kila mmoja kutimiza wajibu ili kwenda sawa na malengo yake.

“Mwenzangu di nzuri sana hapa, hii ni changamoto kwangu na lazima niendeleze mazuri yote aliyoyafanya hapa na ndio maana niliushawishi uongozi kubaki naye hapa kunisaidia kuelewa mambo kadhaa ya klabu,” alisema Lwandamina.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia alisema kuwa anatambua Yanga ni timu kubwa yenye mashabiki wengi na kwa kupitia taaluma yake atahakikisha anaendeleza furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo.

54 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*