Yanga kuingia kambini Nov 25

meandikwa na Vicky Kimaro

IKIWA imejipanga kuhakikisha inaanza vema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kikosi cha Yanga kitaingia rasmi kambini wiki ijayo Novemba 25.

Habari ambazo Habari Leo imezipata zinadai kuwa kikosi hicho huenda kikaweka kambi nje ya nchi kujiandaa na ligi.

Tayari kocha mpya wa klabu hiyo, George Lwandamina amependekeza wachezaji wawili wasajiliwe dirisha hili dogo, ambao ni kiungo wa ulinzi Mzambia Meshack Chaila na mshambuliaji Mkenya Jesse Were ili kuimarisha kikosi hicho.

Chaila na Were wote walikuwa wachezaji tegemeo wa kocha Lwandamina katika kikosi cha Zesco United kilichofika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu kabla ya kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyofanikiwa kutwaa taji hilo.

Yanga imekuwa na tatizo la kiungo mkabaji na hilo waliligundua wakati wakishiriki michuano ya klabu bingwa Afrika.

Tayari kuna taarifa kuwa Yanga imeshamalizana na wakala wa wachezaji hao siku yoyote kuanzia leo watatua nchini kwa ajili ya kumwaga wino tayari kuichezea timu hiyo ya mtaa wa Jangwani.

Lakini Yanga italazimika kukata wachezaji wawili wa kigeni ili kuwasajili Chaila na Were kwa sababu tayari imekwishatimiza idadi ya wachezaji saba wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu.

Wachezaji wa kigeni wa Yanga kwa sasa ni mabeki Mbuyu Twite kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Vincent Bossou kutoka Togo, viungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda, Thabani Kamusoko, washambuliaji Donald Ngoma kutoka Zimbabwe, Obrey Chirwa kutoka Zambia na Amissi Tambwe kutoka Burundi.

Hata hivyo imeelezwa kuwa Twite ambaye mkataba wake wa miezi sita umefikia tamati huenda akafungashiwa virago ndani ya klabu hiyo huku Bossou akatolewa kwa mkopo huku Chirwa naye akiwa kwenye hati hati kwa vile ameshindwa kuonesha uwezo wake tangu atue ndani ya klabu hiyo ya Jangwani na kushindwa kuwapiku Amis Tambwe na Donald Ngoma.

Lwandamina amechukua nafasi ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyeongoza Yanga kwa awamu mbili tangu mwaka 2014. Inadaiwa wasaidizi wa Pluijm, Juma Mwambusi (Kocha Msaidizi), kocha wa makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Mtunza Vifaa vya timu, Mahmoud Omar ‘Mpogolo’ na Dk Edward Bavu pia wataondoka na Lwandamina atasaidiwa na wazalendo Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.

Pluijm anaondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 128, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23.

Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014 baada ya kumrithi Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts, Pluijm alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana alipomrithi Mbrazil Marcio Maximo, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.

Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit alipoulizwa kuhusu suala la usajili alisema kwa kifupi, “Sijui lolote, Kamati ya Usajili ndio yenye mamlaka ya kuzungumzia mambo ya usajili na ndio inajua nani anasajiliwa kwa mapendekezo ya mwalimu au la.”

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*