Shein aridhishwa na utekelezaji wa bajeti

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema ameridhika na utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2016-2017.

Dk Shein alisema hayo wakati akikamilisha kikao cha kupitia Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ kilichofanyia jana, Ikulu.

Alibainisha kuwa hatua hiyo ni matokeo ya umakini katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi bora wa matumizi ya serikali kwa kuziba mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.

Dk Shein alifafanua kuwa hadi sasa ambapo tayari wizara 11 kati ya 13 zimeshawasilisha taarifa zao za utekelezaji wa shughuli za serikali, utekelezaji wa bajeti uko juu ya asilimia 75.

Alieleza kuwa mwelekeo wa serikali hivi sasa ni kuendelea kuchukua hatua zaidi ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi ya serikali ili kutekeleza shughuli za serikali kama zilivyopangwa.

Katika kikao hicho ambapo kilihusu utekelezaji wa kazi za Idara Maalum za SMZ, Dk Shein alirejea ahadi yake ya kuhakikisha maslahi ya watumishi wa idara hizo yanafanana na yale ya vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliwapongeza watumishi wa idara hizo kwa kutekeleza majukumu yao ya kulinda amani na utulivu Zanzibar kwa kushirikiana na vikosi vingine vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akitoa maelezo katika kikao hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ Haji Omar Kheri alieleza kuwa Wizara yake katika mwaka huu wa fedha inatekeleza miradi minne.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Zanzibar Salama, Mradi wa Ujenzi wa Vituo vya Uzamiaji na Uokozi, Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Mama Wajawazito na Watoto katika Hospitali ya KMKM Kibweni na mradi wa ujenzi wa Gereza la Watoto.

Aidha alieleza kuwa wizara yake katika kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka huu ilipangiwa jumla ya Sh bilioni 20.763 ambapo hadi mwezi Septemba, fedha zilizopatikana ni Sh bilioni 18.16 sawa na asilimia 88.

82 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*